Sunday, August 10, 2008

IJUE SIRI YA BOYFRIEND NA GIRLFRIEND 4

MAANA ILIYOFICHIKA YA GIRLFRIEND NA BOYFRIEND

Nataka ujue maana ya girlfriend na boyfriend, kama jinsi Shetani anavyoitumia, na jinsi anavyochochea tafsiri yake ndani ya watu wengi na kuwaangusha katika zinaa (dhambi)

Kwa maana ya ndani iliyofichwa na kufunikwa kwa maneno mazuri yaani girlfriend na boyfriend, ni hii; Ni uhusiano wakaribu sana kati ya watu wa jinsi tofauti na mara nyingi huambatana na kufanya ngono (zinaa)

Vijana wengi hawaukubali ukweli huu, na ndiyo maana nikakuuliza unapata hisia gani unaposema girlfriend au boyfriend wangu, tofauti na uposema rafiki yangu kwa hali ya kawaida? Kama na wewe unaipinga maana hiyo niliyokuambia fanya hivi; Jaribu kumuuliza msichana mwenye akili timamu kama anaye girlfriend, au muulize mvulana ambaye ni rafiki yako akuambie kama anaye boyfriend. Nina uhakika hatakupa jibu la moja kwa moja na ukipigwa usishangae, na usiseme Adriano amenituma.

Vijana wengi hupenda kuwa na girlfriend au boyfriend wakiwa na maana ya urafiki wa kawaida, wakipendana, wakisaidiana na kushirikiana mambo mbalimbali mazuri. Sikiliza uhusiano huu hauna asili ya Afrika na asili yake ni nchi za magharibi (western countries) na kwao huu hi uhusiano wenye lengo la kufanya ngono na hutoa nafasi ya wazi kabisa ya kufanya zinaa. Girlfriend au boyfriend si mchumba na wala si mke.

Ooh! Haleluya! Inawezekana hata maana ya mchumba hufahamu. Sikiliza mpendwa; Mchumba ni mtu wa jinsia tofauti na wewe ambaye umemposa au umeposwa naye na tena umefanya naye shauri au patano au mkataba au agano kuwa utaoana naye. Na baadaye patano hilo hufanyika mbele ya mashahidi (wazazi, jamaa, marafiki na kanisa) Na huyo huwa ni matunda ya maombi yako kwa BWANA akupatie. Maana yake ni kwamba, unakuwa umefunga mlango wa watu kukuchumbia au wewe kumchumbia mtu mwingine. Biblia inamwita mtu aliyeposwa mke na yule aliyeposa Biblia inamwita mume. Usifikiri ni jambo la kujiamulia tu utakavyo wewe, upo utaratibu wa Mungu. Urafiki wa uchumba haufanani na urafiki wa girlfriend na boyfriend, hivyo mchumba si girlfriend au boyfriend. Na pia girlfriend au boyfriend si machumba. Wengi wenye girlfriend au boyfriend ukiwauliza, kama wana mpango wa kuoana wanajibu Mungu akipenda. Sikiliza, utaratibu wa Mungu juu ya ndoa sio wa kubahatisha.

Natamani sana utambue kuwa Shetani ndiye mwanzilishi wa girlfriend na boyfriend. Na kwa kupitia maneno hayo au uhusiano huo hupenyeza hisia na misisimko ya dhambi ndani ya mioyo ya watu, ambayo hupingana na neno la Mungu; msiyachochee wala kuyaamsha mapenzi. Maana girlfriend na boyfriend ya kawaida huwa haina ubaguzi, kwamba huyu ni girlfriend au boyfriend wangu na huyu sio.

Hivyo kutokana na mahusiano haya automatically mapenzi huchochewa na kuamshwa. Hali ya kuwa na boyfriend au girlfriend humpa Ibilisi nafasi ya kupenyeza tamaa za mwili. Maana kila mmoja hutamani kuwa karibu sana na mwenzake. Na mara nyingi hupenda kufanyiana mambo mazuri wakimaanisha upendo. Likini ukweli ni kwamba, Shetani hufunga ufahamu wao rohoni na macho yao ya kiroho hutiwa giza na hujikuta wakiivunja amri ya sita. (usizini) Asilimia kubwa ya vijana walio na magirlfriend au maboyfriend wamekwisha fanya uzinzi na kama bado hawajafanya ndani ya mioyo yao hivi sasa kuna shauku kubwa ya kutaka kufanya hivyo na huanza kushindwa kujizuia wanapokuwa pamoja. Ooh, Roho Mtakatifu akusaidie! Na kama hawatamruhusu Yesu aingie ndani ya mioyo yao , wataanguka katika zinaa iwapo uhusiano huo utaendelea.

Jiulize Biblia inaeleza wapi uwe na girlfriend au boyfriend? Biblia inasema “Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote na huo utakatifu ambao hapana mtu atakayemwona Bwana asipokuwa nao” Ebrania 12:14 Maana yake uwe rafiki wa watu wote, na sio kuwa na special friend yaani girlfriend au boyfriend, na kama ni special basi awe ndiyo ambaye Mungu amekupa kuwa mke au mume na uwe na uhakika. Hata hivyo ukaribu wenu una mipaka yake.

Mtume Paulo aliandika hivyo akimaanisha urafiki hasa kati ya wavulana na wasichana. Kama huamini soma misitari unaofuata baada ya huo Ebr 12:15-16 anasema hivi; “mtu asiipungukie neema ya Mungu” maana yake mtu asitoke katika mpango ambao Mungu amempangia, ambao ni kwa neema tu mtu hupewa. Halafu anasema, “shina la uchungu lisije likachipuka na kuwasumbua” maana yake hisia za ndani ambazo mwisho wake ni uchungu (jehanamu) zisiwasumbue. Sikiliza; mahusiano haya mara nyingi husababisha chuki, mafarakano, vijana wengi wana uchungu mioyoni mwao na wakati mwingine hupelekea baadhi ya vijana kujiua. Wapo vijana ambao wamejeruhiwa mno, na ukimwambia suala la kuoa au kuolewa anatamani akumalize kabisa, maana hataki kusikia, na hiyo ndiyo furaha ya Shetani unapokuwa katika hali ya namna hiyo. Ndiyo maana Paulo anaendelea kusema; “asiwepo mwasherati…” Maana girlfriend na boyfriend huchipusha shina la uchungu, husumbua na mwisho wake ni uasherati. Shina la uchungu linapochipuka humtia mtu unajisi (humchafua kiroho), Ebr 12:15. Kumbuka girlfriend au boyfriend sio mchumba, sio mke ana jinsia tofauti na wewe na ana hisia za mwili kama kawaida.

Vijana wengi wanajua kuwa uhusiano huu huchochea kufanyiana mambo ambayo Mungu hakuruhusu kufanyika kwa wakati huo, na hii ni kwa sababu Shetani hupata nafasi. Haijalishi unataka au hutaki, unapokuwa na girlfriend au boyfriend, Ibilisi hutumia nafasi hiyo kuingiza hisia za dhambi ndani ya moyo wako na kutia giza macho yako ya kiroho ili usiione njia ya Bwana. Mithali 16:2 “njia zote za mtu ni safi machoni pake mwenyewe, bali Bwana huzipima roho za watu” Hivyo ni lazima uwe na uhakika kuwa unaongozwa na Roho Mtakatifu. Rumi 8:14 “Kwa kuwa wote wanaoongozwa na Roho wa Mungu hao ndiyo wana wa Mungu”

Mwanzoni vijana wengi walipokuwa na girl/boyfriend zao, hawakupenda sana kuonekana na watu (maana matendo ya giza hayafanyiki nuruni), lakini siku hizi wapo wengi ambao hupenda kuonekana kuwa wana girlfriend au boyfriend. Na lengo ni kuonekana kuwa wao ni wa kisasa sana au ni kuonesha kuwa ana handsome mzuri na kama ni kaka basi anataka watu wamuone beauty girl wake, siku hizi wanawaita sex lady. Hii ni roho ya Shetani ya kiburi na kwa tafsiri nyingine moyo wake umekuwa mgumu. Mara nyingi hupenda kukaa aidha gizani, uchochoroni kwenye kona au chumbani wao wawili. Hii ni kujitafutia mazingira ya kufanya zinaa, maana ndio mpango wa Shetani kusababisha kuwapo kwa uhusino wa namna hii. Maana yeye hupinga neno la Mungu, 1 Kor 6:18 “Ikimbieni zinaa” Biblia haisemi kemea zinaa bali inasema kimbia, maana yake uondoke kabisa karibu na zinaa.

Mkumbuke Yusufu alivyofanya kule misri kwa mke wa Potifa. Mwanzo 39:5-12 “…nitafanye ubaya huu mkubwa nimkose Mungu…, Yusufu akaiacha nguo yake mikononi mwake akakimbia akatoka nje”

Wengine hupenda kubusiana 2 Kor 13:12, “Salimianeni kwa busu takatifu” Hili si busu kwa boyfriend au girlfriend maana huwa linaambatana na hisia ya dhambi (ngono). Na huwezi kusalimia kwa busu takatifu kama wewe si mtakatifu.

Wengine hupeana zawadi. Kupeana zawadi si tatizo ila tatizo ni aina ya zawadi wanazopeana na malengo hasa ya kutoa zawadi hizo. Kwa mfano mtu anakupa zawadi ya nguo ya ndani (underwear) au picha za uchi, hii ni ishara ya kukutaka ngono. Kwa hiyo kupeana zawadi ni vema iwapo zawadi hiyo inatolewa katika mpango wa Mungu na sio kwa ajili ya kupata kitu fulani au kwa ajili ya anasa. 2 Timotheo 3:4b “Wapendao anasa kuliko kumpenda Mungu”

Wengine hujiwekea maagano kwa matendo au maneno yao wenyewe. Sikiliza; mtu anasema bila wewe sina raha, ni wewe tu unayenifurahisha au siwezi kuishi bila wewe n.k. Maneno haya hufanyika kuwa agano au mkataba katika roho na hupelekea kukosa amani, kukosa furaha na wakati mwingine hupelekea kifo pale urafiki unapokwisha. Hii ni kwa sababu maneno hayo hutamkwa lakini huwa ni unafiki au ni nje ya mpango wa Mungu. Pia huwa rahisi kwa Shetani kuwaangusha maana huwa hakuna uongozi wa Roho Mtakatifu. Jaribu kujiuliza kwa nini usiseme, bila Yesu sina raha au ni Yesu tu unayenifurahisha au siwezi kuishi bila Yesu? Maana huo ndio ukweli. Mithali 6:2 “Basi umetegwa kwa maneno ya kinywa chako, umekamatwa kwa maneno ya kinywa chako” Pia katika maneno ipo nguvu kubwa kiasi cha kuweza kusababisha kifo. Mith 18:21a “mauti na uzima huwa katika uwezo wa ulimi”

Kuwa na girlfriend au boyfriend si mpango wa Mungu. Kwa nini uhangaike kuwa na girlfriend na boyfriend wakati watu wote ni rafiki zako? Ndivyo yasemavyo maandiko, “Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote” Ikiwa ni wakati wa kuwa na partner, ni vema kupiga magoti na kumwomba Mungu akupe ambaye ni mwenzi wako mtarajiwa.

Wengine huwa na girlfriend au boyfriend kwa malengo ya kuja kuoana baadaye. Na wengine huwa na marafiki wa aina hiyo wengi ili aweze kuchagua mmoja anayefaa. Ooh Skiliza, hakuna kitu cha namna hiyo katika maandiko matakatifu. Mungu humpatia mtu mwenzi mmoja na kamwe Biblia haisemi kuwa Mungu atakuletea wasichana au wavulana wengi ili uchague mmoja, huo ni utaratibu wa Shetani maana yeye ndiye hubahatisha ila Mungu wetu hafanyi mambo kwa kubahatisha. Mith 19:14 “…bali mke mwenye busara, mtu hupewa na BWANA”

Ngoja nikupe mifano kutoka kwenye Biblia ili unielewe vizuri;

Isaka alipotaka kuoa alitafutiwa mke na sio girlfriend na wala hakuwa na girlfriend hapo mwanzo. Mwanzo 24. Utaratibu wa kwenda kumtafuta mke wa Isaka kutoka kwa jamaa ya Baba yake ni kivuli cha mambo ya sasa. Maana yake ni sawa na kijana kupiga magoti mbele za Mungu kuomba mwenzi wa maisha. Maana Mungu ndiye Baba yetu, ndiyo maana tunaomba mwenzi (mke/mume) kutoka kwa jamaa ya Mungu kama vile Isaka alivyotafutiwa kutoka kwa jamaa ya Baba yake.

Hatupigi magoti mbele za Mungu kuomba girlfriend au boyfriend bali tunaomba Mungu atuwezeshe kuwa na amani na watu wote. Na kama ni kuoa au kuolewa tunaomba mwenzi na si vinginevyo. Kumbuka Biblia yatuagiza kuomba sawasawa na mapenzi ya Mungu. Ni lazima kwanza usome neno la Mungu na umruhusu Kristo akae ndani ya moyo wako ili akupe Roho Mtakatifu ambaye atakuwezesha kuomba sawasawa na mapenzi ya Mungu. Rumi 8:26 “Kadhalika Roho naye hutusaidia udhaifu wetu, kwa maana hatujui kuomba jinsi itupasavyo...” Ndiyo maana ni lazima kukubali Yesu akuokoe na akupe ufahamu wa rohoni na nguvu ya kuomba ili uelewe undani wa uhusiano wako ulio nao sasa (kama unaye), je watoka kwa Mungu au ni mawazo yako tu.

Yakobo alipotaka kuoa, alikwenda kwenye ukoo wa mama yake akajipatia wake na si girlfriend na wala Biblia haituambii kuwa alikuwa na girlfriend hapo mwanzo.

Wengi hujikuta wakifanya ngono aidha kwa kutaka au pasipo kutaka, lakini chanzo halisi ni boyfriend au girlfriend wake. Na vijana wengi hujuta na hulaumiana baada ya kufanya dhambi. Nimewasikia wengine wakisema, “Sikuwa nataka kufanya ngono lakini kila ninapokuwa na girlfriend/ boyfriend wangu najikuta tu nimekwisha fanya hivyo, sijui kwa nini?” Kumbuka nimekuambia kuwa yapo mambo ambayo Biblia hairuhusu kufanyika kwa wakati huo. Lakini mtu anapokuwa na boyfriend au girlfriend wake hufanya hivyo. Na mwili una mihemko yake na pia kwa kuwa hukutii maandiko ( Ikimbieni zinaa) na pengine huna Roho Mtakatifu, hivyo huongozwa na mwili wako na sio Roho wa Mungu.

Wengine kwa kigezo cha kuonesha upendo kwa mwenzake, hupenda kushikana shikana, kutomasana, kukumbatiana, kupigana busu, kupakatana au kusemeana maneno kama niliyokutajia hapo mwanzo. Kwa nini hufanya hivyo? Kwa sababu ni girlfriend au boyfriend wake. Mith 7:10, 13, 21 “Natazama mwanamke akamkuta, ana mavazi ya kikahaba, mwerevu wa moyo. Basi akamshika, akambusu, akamwambia kwa uso usio na haya. Maneno yake mengi na ulaini akamshika kwa ubembelezi wa midomo yake akamshinda” Ndio maana nikakwambia kwamba, hata kama ni mchumba, ukaribu wenu una mipaka yake, na pasipokua na kiasi hupelekea kufanya dhambi na matatizo mengine makubwa katika jamii na hulichafua kanisa (kwa vijana walio makanisani).

BOYFRIEND NA GIRLFRIEND ZILIANZAJE?

Hebu jiulize kwa nini mtu awapo na boyfriend au girlfriend wake hupenda kufanyiana mambo niliyokutajia hapo juu? (kubusiana, kukumbatiana, kutomasana au kusemeana maneno niliyokutajia). Zipo sababu zilizopelekea kufanyiana mambo hayo, nayo ni hii; Ni kutafuta amani, furaha na upendo uliopotea. Inawezekana unajiuliza ulipotea wapi au inakuwaje? Ninachotaka ni wewe ufahamu ni nini chanzo cha kuwepo kwa girlfriend na boyfriend.

Pendo la Mungu ni pendo la AGAPE. Ni pendo ambalo halidai malipo wala halihesabu gharama. Ni upendo ambao hudhihirika wazi kwa matendo yake na sio kwa maneno tu. Ni pendo lililomfanya Mungu kumtoa mwana wake wa pekee Yesu kwa ajili yetu.

Mwanadamu ameumbwa kwa mfano wa Mungu, Mwanzo 1 :27 Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimuumba mwanamume na mwanamke aliwaumba. Kwa hiyo mtu akawa na tabia za uungu ndani yake. Basi ni dhahiri kuwa tabia ya upendo wa Agape ilikuwapo ndani ya mwanadamu. Pendo hili la agape kwa mwanadamu likafanyika PENDO LA FAMILIA (Family love)

Pendo la agape, Mungu akampenda mtu ambaye amemuumba, maana ni mtoto wake. Pendo la familia, wazazi wakawapenda watoto wao na watoto wakawapenda wazazi wao. Ni upendo wa asili (natural love) ambao Mungu aliuweka ndani ya mwanadamu.

Katika familia ambazo upendo wa familia umehuishwa na Kristo, pana tabia za namna hii ; ngoja nikumegee kidogo vitu vitamu ;

Mama huwa karibu au humwangalia sana mtoto wa kiume, japo humwangalia pia mtoto wa kike. Maana yake uhusiano wa kifamilia kati ya mtoto wa kiume na mama huwa wa karibu sana. Ndiyo maana mara nyingi mama huwa wa kwanza kugundua na kumwonya mtoto wa kiume anapoanza tabia zisizofaa. Mara nyingine utamsikia mtoto wa kiume akimsifia mama yake ‘Mama ukivaa kitenge hiki huwa unapendeza sana’ au wakati mwingine akimtengenezea mama yake kilemba kikae sawasawa, fuatilia utayona haya.

Vilevile uhusiano kati ya mtoto wa kike na baba yake huwa wa karibu sana. Baba humwangalia au hushughulika sana kwa ajili ya binti yake kuliko mtoto wa kiume, japo pia humwangalia mtoto wa kiume. Uliza watoto wa kiume watakuambia, wengine husema ‘Baba anampendelea sana dada sijui kwa nini’ ni kwa sababu upo upendo wa ziada. Ndiyo maana Baba huwa wa kwanza kugundua tabia fulani kwa binti yake, na ndiyo maana mara nyingi utawasikia akina baba wakiwauliza wake zao, ‘Binti yetu siku hizi vipi, mbona hivi ?’ Baba hujisikia uchungu sana binti yake anapofanya mambo yasiyofaa kuliko mtoto wakiume anapofanya hivyo. Maana yake ni kwamba kuna upendo wa ziada kati ya baba na binti yake.

Fungua Biblia yako, tazama Mwanzo 27 :46 ‘Rebeka akamwambia Isaka, moyoni mwangu sina raha kwa sababu ya hao binti za Hethi, kama Yakobo akitwaa mke katika binti za Hethi, kama hawa binti za nchi, maisha yangu yananifaidia nini ?’ Inaonesha wazi kabisa kuwa Rebeka alikuwa na upendo wa ziada kwa mwanawe Yakobo. Kwa tafsiri nyingine alikuwa akitafakari sana juu ya maisha ya baadaye ya kijana wake, (future ya Yakobo) hata akapata uchungu sana moyoni mwake (anasema, maisha yangu yananifaidia nini)

Angalia upendo wa Hana kwa mwanawe Samweli, 1 Sam 2 :19 ‘tena mama yake humfanyizia kanzu ndogo na kumletea, mwaka kwa mwaka…’ Kumbuka Samweli alikuwa akihudumu Hekaluni, kwa hiyo hakukuwa na haja sana ya mama yake kumfanyizia kanzu, maana Hekaluni mna mavazi.

Kibiblia maana yake ni hii ; Mtoto wa kiume anapokuwa bado hajaoa, ndani ya moyo wake, nafasi ambayo itakuwa ya mkewe huwa inashikiliwa na mama yake. Na kabla mtoto wa kike hajaolewa, nafasi ambayo itakuwa ya mume wake hushikiliwa na baba yake. Na jambo hili hushikiliwa na family love. Ndivyo ilivyo usishangae, ngoja nikupe mifano kutoka kwenye biblia ;

Kabla Isaka hajaoa nafasi ya mkewe ndani ya moyo wake ilikuwa inashikiliwa na mamaye Sara. Lakini Sara alifariki kabla Isaka hajaoa. Isaka alihuzunika sana, hakuwa na furaha na mara nyingi alikuwa akitafakari peke yake. Hii inaonesha jinsi upendo kwa mama yake ulivyokuwa wa ziada. Ndipo mtumishi wa Ibrahimu alipotumwa kumtafutia Isaka mke. Mwanzo 24 :24…, ‘…bali nenda hata nchi yangu, na kwa jamaa zangu, ukamtwalie mwanangu, Isaka mke’ Mara baada ya Isaka kumwona Rebeka, ghafla huzuni ikaisha, furaha ikarejea, akafarijika. Mwanzo 24 :67 ‘Isaka akamuingiza Rebeka katika hema ya mama yake, Sara, akamtwaa Rebeka akawa mkewe, akampenda, Isaka akafarijika kwa ajili ya kufa kwa mamaye’

Biblia inasema, Isaka akamwingiza Rebeka katika hema ya mama yake, maana yake, ndani ya moyo wa Isaka palikuwa na nafasi iliyokuwa wazi, ambayo imeachwa na mama yake baada ya kufariki. Sasa Rebeka anaingizwa katika nafasi hiyo. Unaweza kujiuliza kwa nini asimwingize kwenye hema ya baba yake ? Usifikiri alimwingiza kwenye hema ya mama yake eti kwa sababu mama yake alikuwa amefariki, la hasha sivyo. Mambo au desturi nyingi katika Agano la Kale ni kivuli cha mambo ya sasa. Hivyo maana yake ni kumwingiza Rebeka moyoni mwake. Ndivyo ilivyo, maana anachukua nafasi ambayo hapo mwanzo ilishikiliwa na mama. Wimb 3 :4 ‘…nikamwona mpendwa wa nafsi yangu, nikamshika nisimwache tena, hata nilipomleta nyumbani mwa mamangu, chumbani mwake aliyenizaa’ Maana yake, mkewe anaingia kwenye nafasi ambayo hapo mwanzo ilishikiliwa na mamaye Sulemani.

Baada ya kujua upendo uliopo katika familia, uelewe kuwa pendo hilo (family love), ndilo lililoshikilia amani na furaha za watoto kabla hawajaoa au kuolewa. Inawezekana unafikiri mambo haya yalikuwa ni desturi zao tu. Umesahau kuwa mambo ya Agano la Kale ni kivuli cha mabo ya sasa ? Soma kitabu cha Waebrania sura ya kumi, utaelewa.

1 comment:

Unknown said...

hongera sana Dr kwa kufikia hapo ambapo umefika. mambo haya ni muhimu sana kwa vijana wa wakati wa leo. kwa kuwa wengi hawaelewi gf na bf ina maana gani. wengi hufikiri ni wapenzi wa ngono na hili limeahribu sana vijana na mabinti wengi. Mungu akubariki sana
Pastor Nkya