Sunday, August 10, 2008

IJUE SIRI YA GIRLFRIEND NA BOYFRIEND-3

MAPENZI

Mapenzi ni kitu kilichowekwa na Mungu ndani ya kila mwanadamu. Mapenzi ni kitu kilicholala na huamka yenyewe kwa wakati ambao Mungu amepanga kwa kila mtu. Hivyo mapenzi yapo ndani ya kila mtu tangu anapozaliwa, ila huwa yamelala, na yana muda wake wa kuamka. Wimbo 2 :7 “Nawasihi enyi binti za Yerusalemu,… msiyachochee mapenzi wala kuyaamsha, hata yatakapoona vema yenyewe” Utakubaliana nami kuwa huwezi kuamsha kitu ambacho hakijalala, kwa hiyo mapenzi huwa yamelala. Anaposema ‘yatakapoona vema yenyewe’ maana yake Mungu alikwisha yapangia utaratibu na muda wake ili yaamke. Kumbuka kila kitu alichokifanya Mungu ni kizuri na chema hivyo alijua hali halisi ya ujana, hali yetu ya kibayolojia ndiyo maana akaweka muda wa mapenzi kuamka. Biblia inasema mapenzi huweza kuamshwa na mtu mwenyewe. Wimbo 2 :7 “…enyi binti za Yerusalemu,…msiyachochee mapenzi wala kuyaamsha…” Maana yake wewe mwenyewe unao uwezo wa kuyachochea na kuyaamsha. Inawezekana ukafikiri ni sawa au ni vema tu kuyachochea na kuyaamsha mapenzi wakati wowote, lakini jiulize kwa nini Mungu aliyawekea utaratibu (gerentee) ya muda maalumu wa kuamka ? Sikiliza, Mungu amevipa vitu vyote kufanywa kwa muda aliyepanga yeye kwa sababu vitu hivyo huwa vizuri vinapofanyika kwa muda huo. Ooh ! Haleluya ! Unapofanya kitu chochote hata kama ni kizuri ukikifanya kwa muda usio wa Mungu kitu au jambo hilo linakuwa si jema tena linakuwa dhambi, na haliwi lenye faida. Muhubiri 3 :1,9-11 Kwa kila jambo kuna majira yake na wakati wa kila kusudi chini ya mbingu, …je mtendaji anayo faida gani katika yale anayojishughulisha nayo ? Nimeona taabu ambayo Mungu amewapa wanadamu, ili kutaabika ndani yake. Kila kitu amekifanya kizuri kwa wakati wake, ila kwa jinsi mwanadamu asivyoweza kuivumbua kazi ya Mungu anayoifanya tangu mwanzo hata mwisho”

Lazima ujue kuwa Mungu alikwishaandaa mpango na utaratibu mzuri wa maisha yako tangu enzi. Isaya 46 :10 “Kumbuka mambo ya zamani za kale maana mimi ni Mungu wala hapana aliye kama mimi, nitangazaye mwisho tangu mwanzo na tangu zamani za kale mambo yasiyotendeka bado, nikisema shauri langu litasimama, nami nitatenda mapenzi yangu yote” Mungu anaposema nitangazaye mwisho tangu mwanzo, maana yake aliufahamu mwanzo wako hata mwisho wako. Alijua utazaliwa lini, utazaliwa wapi na nani na alijua utaoa au utaolewa lini na nani na utaishi wapi. Na katika yote hayo Mungu anakuwazia mawazo mema na mpango wake juu maisha yako ni mwema. Ni lazima uelewe hili, Mungu anaposema, shauri langu litasimama maana yake anategemea yote aliyokupangia, ukikubali na kutii yote akuagizayo, hataacha kutimiza yote aliyokupangia ambayo ni mema (maana hakukupangia jambo baya), mazuri na mwisho wake ni uzima wa milele.

Sikiliza mpendwa, Mungu humaliza kwanza halafu ndipo anaanza. Ooh ! Haleluya ! Maana yake ni hii yeye aliratibu maisha yako na kukupangia matukio yote hata mwisho, akaona ni vema ndipo akaruhusu uwepo duniani. Tatizo kubwa ni watu kutojua na kutotaka kujua kalenda ya Mungu kwao na hivyo hutafuta njia za mkato (shortcut ) na ndipo uangamivu huja juu yao. Yer 29 :11 Maana ninajua mawazo ninayowawazia nnyi asema Bwana, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumiani siku zenu za mwisho »

Kukuwazia amani, maana yake ni kuwa na maisha mazuri ya furaha hapa duniani. Na anaposema ‘kuwapa ninyi tumaini la siku zenu za mwisho’ uwe na uhakika ni uzima wa milele. Hivyo hata utaratibu wa mapenzi upo ndani ya mpango wa Mungu. Watu wengi husumbuka kutafuta utaratibu wao badala ya kumwachia Mungu awaongoze katika utaratibu ulio mzuri na ulio bora.

Vijana wengi hushindwa kuishi sawasawa na mpango wa Mungu aliowapangia, na wengi wao si kwa sababu hawataki ila ni kwa sababu hawaijui siri hii kubwa ambayo Mungu ameiweka ndani yao. Unauliza siri ipi, soma Muh 3 :11 Kila kitu amekifanya kizuri kwa wakati wake, tena ameiweka hiyo milele ndani ya mioyo yao ,… Ni vema uitambue siri hii itakusaidia.

Kwa hiyo mapenzi yamewekewa muda wake wa kuamka, kwa hiyo ukiyaamsha kwa muda wako unaotaka wewe, unakuwa umejitoa katika utaratibu au mpango wa Mungu na kuiendea njia yako binafsi, ambayo mwisho wake ni dharau ya milele yaani Jehanamu. Mara nyingi baada ya vijana kutoka katika mpango wa Mungu na kukutana matatizo makubwa na mazito katika maisha yao hujaribu kuyatatua kwa kutumia akilia zao. Na mara nyingi hufanya maamuzi yasiyo sahihi na hivyo hupata matatizo makubwa zaidi na kusahau kumtegemea Yesu aliye mshauri wa ajabu na mfalme wa amani.

Sikiliza, Uhusiano wowote ni lazima uanzishwe na Yesu mwenyewe ili uhusiano uwe bora, unaompa Mungu utukufu na wenye faida katika maisha yako. Biblia inaeleza jambo hili wazi kabisa, Muh 3 :9 Je mtendaji anayo faida gani katika yale anayojishughulisha nayo ? Ahaa ! Kumbe hakuna faida bali ni hasara tupu kujishughulisha upendavyo wewe na sio kama apendavyo Mungu.

Ndugu mpendwa, hupaswi kuyachochea wala kuyaamsha mapenzi. Inawezekana unatenda matendo au unazungumza maneno ambayo hufanya mapenzi ya wengine kuamka, maana yake umeyachochea, na hii ni chukizo kwa Bwana. Pengine hufanyi ngono lakini umekuwa ukiwafanya wengine waendelee kufanya hivyo. Maana yake ni kwamba unatumiwa na Shetani kama ajenti wake. Inawezekana unajiuliza utayachocheaje mapenzi ya wengine kuamka ? Tembea yako, tazama yako, uvaaji wako, maneno yako na matendo yako yanaweza kabisa kuchochea mapenzi ya wengine kuamka. Ooh, hilo ni somo jingine, Mungu akipenda tutajifunza.



MAANA YA GIRLFRIEND NA BOYFRIEND

Kwanza tuangalie maana halisi ya kawaida ya girlfriend na boyfriend, halafu tuangalie maana halisi anayoitumia Shetani, ambayo imefunikwa kwa maneno mazuri yaani girlfriend na boyfriend, kama mtu awekavyo chakula kizuri katika mtego wa panya.

Neno friend lina maana rafiki, girl ni msichana na boy ni mvulana. Sasa ukiyaunganisha maneno hayo, unapata rafiki wa kike au rafiki wa kiume. Hii ni maana ya kawaida ya girlfriend na boyfriend, si mbaya kwa jinsi unvyoyasikia maneno hayo. Kumbuka Shetani hutumia maneno mazuri akiwa na maana au kusudi la kwake tofauti ambalo ni chukizo kwa Mungu. Na huwateka watu wasipofahamu undani halisi na wasio na macho ya kiroho yaani ufahamu wa rohoni wa kutambua mbinu za Ibilisi. Jambo kubwa hapa si kuvijua vitu au kuyaelewa maneno yanayotajwa, ila ni kufahamu maana halisi ya hayo unayoyasikia katika ufahamu wa rohoni. Haleluya! Ndiyo maana ipo karama ya kupambanua roho.

Mpendwa ni vema uwe makini sana na kila unalolifanya. Wapo watu wanaotetea uovu wakidai wana ufahamu wa roho au wamefunuliwa na roho. Sikiliza, kuwa na roho au kufunuliwa mambo fulani na roho si tatizo, ila tatizo ni roho ya namna gani uliyonayo au ni roho wa nani aliyekufunulia unayotuambia. 1 Yohana 4:1 Wapendwa msiiamini kila roho bali zijaribuni hizo roho, kwamba zimetokana na Mungu; kwa sababu manabii wa uongo wengi wametokea duniani.

Mara nyingi Shetani hutumia maneno mazuri, kumbuka alivyomjaribu Yesu. Mathayo 4:6 Akamwambia, ukiwa ndiwe mwana wa Mungu jitupe chini, kwa maana imeandikwa atakuagizia malaika zake; na mikononi mwao watakuchukua, usije ukajikwaa mguu wako katika jiwe. Haya ni maneno mazuri na pia ni kweli yameandikwa, soma Zaburi 91:11-12 Kwa kuwa atakuagizia malaika zake... mikononi mwao watakuchukua; usije ukajikwaa mguu wako katika jiwe. Lakini ulikuwa ni mtego wa kumtaka Yesu awe na kiburi ili ajikweze au ajitukuze kuwa yeye ndiye mwana wa Mungu. Bwana Yesu aliitambua maana halisi au maana ya ndani iliyifichika, kwa kupambwa kwa maneno mazuri aliyoyataja Shetani, na ndiyo maana Yesu alishinda. Kushinda kwa Yesu si kwa sababu ya kuyaelewa maneno ya Shetani bali ni kufahamu maana ya maneno yale kwa tafsiri ya rohoni. Kwa hiyo huwezi kuona ubaya wa kuwa na girlfriend au boyfriend usipokuwa na ufahamu wa rohoni ambao ndiyo unaotuwezesha kutambua maana halisi zilizofichika.

Hebu jiulize mwenyewe; Unaposema girlfriend au boyfriend wangu ndani yako, moyoni mwako huwa unajisikiaje, unapata hisia gani na huwa unafikiri nini hasa akilini mwako unapotamka hivyo?

No comments: