Sunday, August 10, 2008

IJUE SIRI YA GIRLFRIEND NA BOYFRIEND -5

IMEKUWAJE KUKAWA NA GIRLFRIEND NA BOYFRIEND ?

Shetani mara zote huwa ni muharibifu, huwa analivunja pendo la Agape ndani ya mioyo ya watu, yaani FAMILY LOVE. Kitu cha ajabu kabisa wazazi na watoto ghafla wanakuwa maadui. Na hii mara nyingi ilitokea kutokana na wazazi kufanya maagano na miungu au mizimu (mizimu ni mapepo au roho za Ibilisi zilizovaa sura za watu waliokwisha kufa) au kwa maneno mabaya ambayo huondoa pendo la kweli ndani ya familia. Hii ni ngumu kidogo kwa mtu kuelewa kwa wepesi, ngoja nikuvunjie vipande vidogo vidogo;

Watu walimwacha Mungu na kuzisikiliza roho zidanganyazo, yaani uchawi, mapepo, na mizimu halafu uadui na chuki ikajengeka katika familia. Kwa mfano; Mtu anapiga ramli, mchawi au mganga anamwambia umelogwa na dada yako au mama au baba yako. Wakati mwingine mapepo husema uongo kupitia mtu mmojawapo katika familia hiyo akionekana ni mzima tu au wakati mtu huyo akiombewa na hivyo kuibua uadui, chuki na mafarakano katika familia hiyo. Wakati mwingine Shetani huwafunga watu kwa ulevi na hivyo kupelekea kuvunjika kwa family love. Maana ulevi ni kinyume na agizo la BWANA. Efeso 5:18 “Tena msilewe kwa mvinyo ambamo mna ufisadi; bali mjazwe Roho”

Kutokana na uadui ulioibuka ndani ya familia, kulikosababishwa na watu kufuata njia zao na si njia ya Bwana, matokeo yake ni wazazi na watoto kuwa maadui. Baba anarudi nyumbani amelewa, binti yake anakimbilia jikoni, watoto wa kiume hawakai nyumbani wanazurura tu, kisa mama makali. Wazazi wakakosa busara, hekima na maarifa ya kuwaelekeza watoto wao mambo mema, kwa kuwa wamemwacha Mungu. Na hivyo watoto wao hawakufundishwa na Bwana, Isaya 54:13 “Na watoto wako wote watafundishwa na Bwana; na amani ya watoto wako itakuwa nyingi” Zile sehemu au nafasi za wazazi ndani ya mioyo ya watoto wao zikapotea, zikawa tupu. Maana yake upendo, amani na furaha ndani ya watoto zikapotea. Ndiyo maana nilikwambia kuwa, vitendo vya kukumbatiana, kutomasana, kupakatana, kupigana busu na kuambiana maneno fulani kati ya girlfriend na boyfriend, ni kutafuta amani, furaha na upendo uliopotea. Maana nafasi za wazazi wao ndani ya mioyo yao zipo wazi. Hivyo vijana wakaanza kutafuta namna ya kuzijaza nafasi hizo. Ghafla (special relationship with opposite sex) girlfriend na boyfriend zikaanza. Na vijana wengi wakaingia katika uhusiano wa namna hiyo bila kujua ni nini hasa maana yake na mwisho wake ni nini au ni wapi. Na haikuwezekana kuwa mke kwa sababu umri wao ni mdogo bado na pia haukuwa wakati wa Bwana aliopanga kwa mapenzi kuamka; hivyo vijana wengi baada ya kuingia kwenye mahusiano hayo wakayachochea na kuyaamsha mapenzi, wakajikuta wakifanya zinaa. Hii ikawa kama sehemu ya starehe kujaribu kuiridhisha au kuifurahisha nafsi. Ndiyo maana hakuna uhusiano wa boyfriend na girlfriend kwa watu wazima, ni kwa vijana. Maana sijawahi kuona wazee eti ni boyfriend na girlfriend wake (hata kama hawajawahi kuzaa), kama wapo basi ni mbinu za Shetani kutetea zinaa na hao watakuwa ni watumishi wa Ibilisi.

Sikiliza mpendwa, kubwa analolifanya Shetani ni kuvuruga au kuvunja upendo wa familia. Naye hutumia njia za namna mbalimbali. Njia nyingine anayoitumia Shetani ipo sana katika nchi au mataifa tajiri dunia na sasa njia hii inakuwa kwa kasi sana katika nchi zetu za dunia ya tatu. Anawasogeza wazazi mbali na watoto wao kwa kuwafanya wazazi wajishughulishe sana na pesa na kazi na kusahau wajibu wao kwa watoto wao kama Bwana alivyotuagiza, Wapo BUSY. Waefeso 6:4 “Nanyi akina baba, msiwachokoze watoto wenu; bali waleeni katika adabu na maonyo ya Bwana” Mith 19:18 “Mrudi mwanao, kwa maana liko tumaini; wala usiikaze nafsi yako kwa kuangamia wake” Na ndiyo maana kwa wenzetu (wazungu) mtoto kuwa na girlfriend au boyfriend sio tatizo. Ooh! Roho Mtakatifu akusaidie kuelewa, maana Shetani anatumia nguvu nyingi sana katika kuutetea uovu dunuani.

Inawezekana hunielewi ninaposema ‘anatumia nguvu nyingi’ ninamaanisha nini. Hivi sasa anawatumia watawala, mataifa makubwa na sheria za kimataifa. Ngoja nikupe vitu;

Zipo baadhi ya nchi, mzazi kumwadhibu mtoto ni kosa kisheria, na unaweza hata kufungwa jela. Mnaigeria fulani alikuwa akiishi nchi mojawapo ya Ulaya. Siku moja binti yake alifika nyumbani akiwa na boyfriend wake. Akamtaka baba yake aondoke nyumbani ili yeye apate nafasi ya kustarehe na huyo boyfriend wake. Jambo hilo lilimuudhi sana Baba yake, hivyo alimchapa kofi sawia. Binti yake alipiga simu polisi na baba yake akakamatwa, na akaamriwa kutoonekana mazingira ya nyumbani kwake kwa siku tatu asimsumbue binti yake na kumlipa binti yake kwa kumsumbua na kumzalilisha mbele ya boyfriend wake. Baada ya kesi kwisha akaichukua familia yote na kuirudisha Nigeria .


MATOKEO YA MAMBO YA MWILINI

Baada ya kujua maana ya girlfriend na boyfriend kama jinsi anavyoitumia Shetani, mwanzo wake na lengo la Shetani la kusababisha kuwapo kwa boyfriend na girlfriend, nimeona ni vema pia nikujulishe jinsi mfumo wa mashambulizi ya Ibilisi ulivyo kwa undani zaidi.

Ninataka wazazi na vijana waelewe mbinu hii mbaya mno ya Shetani ambayo huathiri vizazi vingi. Na hata sasa tunahitaji neema ya Mungu na kanisa kusimama katika nafasi yake ili kuokoa vizazi vijavyo kutoka katika hali hii ya zinaa.

Mungu alipomuumba mwanadamu ndani yake aliweka hali ya uungu na akampa mwanadamu jukumu la kuendeleza uumbaji wake, katika mwili na Roho. Mwanadamu huzaliwa katika mwili na pia mtu huzaliwa katika Roho. Yoh 3:6 “Kilichozaliwa kwa mwili ni mwili; na kilichozaliwa na Roho ni Roho”

Mungu ameagiza mwanadamu amwabudu, amsujudie, amheshimu na kumtumikia yeye peke yake. Wazazi wanalo jukumu kubwa la kuwalea watoto wao katika maadili mema sawasawa na mpango wa Bwana. Na hii ni ili watoto wakue wakimfahamu Mungu, wamtii na kumtumikia.

Msingi mzuri wa utumishi na nafasi ya kijana katika kanisa na jamii kwa ujumla huanza kuundwa tangu tumboni (utunzaji wa mimba), anapozaliwa na katika ukuaji wa mtoto (namna mtoto anavyolelewa). Utunzaji wa mimba unahitaji ushirikiano wa wazazi wote wawili, baba na mama pamoja na jamii nzima inayowazunguka. Wazazi walio na hofu ya Mungu na wanaomtii Mungu katika maisha yao, huwa na hekima na ufahamu wa Rohoni, na hivyo huwa na uwezo mkubwa wa kuwalea watoto wao katika misingi mizuri ya Kikristo na maadili mazuri katika jamii nzima. Mungu naye huwa akiwafundisha watoto wa watumishi wake. Isaya 54:13 “Na watoto wako wote watafundishwa na BWANA; na amani ya watoto wako itakuwa nyingi” Watoto wakifundishwa na Mungu huwa watumishi wazuri wa Mungu, huwa waadilifu na wenye manufaa makubwa hasa katika jamii yao . Shetani analifahamu hili, na ndiyo maana huanza kwa kuharibu misingi ya vijana tangu utotoni, maana anajua watamshinda. 1 Yoh 1:14 “Nimewaandikia ninyi,… vijana kwa sababu mna nguvu, na neno la Mungu linakaa ndani yenu, nanyi mmemshinda yule mwovu” Ukisoma maneno haya kwa kutafakari utaona wazi kabisa kuwa hali ilivyo sasa ni kama kinyume. Ooh! Mungu tusaidie vijana. Biblia inasema ‘vijana wana nguvu’ na ndivyo inavyopaswa kuwa. Lakini vijana wengi siku hizi ni dhaifu mno, maana wanamtumikia Shetani. Sasa hivi wengi ndiyo wadhaifu kiroho, afadhali wazee wana nguvu. Biblia inasema ‘neno la Mungu linakaa ndani ya vijana’ lakini vijana wengi wa sasa hawana neno ndani yao . Kinachosikitisha sana ni hiki, ‘vijana wanaambiwa wamemshinda Shetani’ hapa mimi sisemi, jaribu kufikiri kwa makini na kutafakari maisha yako wewe kijana au vijana wengine unaowafahamu. Je wamemshinda Shetani?

Ili familia iwe bora na yenye ufahamu wa Ki-Mungu ni lazima au inahitajika iundwe na Mungu mwenyewe. Uhusiano wa girlfriend na boyfriend mara nyingi umepelekea mimba zisizotarajiwa, mimba nyingine zimetolewa, na zilizobahatika kufikia mwisho hazikupata matunzo mazuri na hata watoto hao mara nyingi hukosa malezi bora. Wakati mwingine mahusiano haya yamesababisha kuwepo kwa ndoa zisizo na hofu ya Mungu kwa kuwa zilianza kimwili hivyo mara nyingi huvuna matendo ya mwili, kama hawakutubu na kumpa Yesu maisha yao .

Kwa kuwa ndoa nyingi zilizoanza kwa namna hiyo, huwa na mafarakano, na mara nyingi huwa na maisha yaliyojaa misongo ya mawazo (stress) kwa sababu ya kuvurugika kwa mipango mbalimbali. Na pengine hutengana na hivyo watoto hukosa malezi bora na mara nyingi huathirika kiafya na kisaikolojia. Na haya yote huchangiwa na ama malezi duni ya mimba ama wakati wa ukuaji ama mazingira magumu au yasiyo na utulivu (family disharmony) au kukosa malezi ya mzazi mmojawapo.

Ngoja nikupe mifano kidogo; Watoto wengi ambao walikuwa na utapia mlo (kwashiorkor) hupata matatizo ya uwezo wa kufikiri wanapokuwa watu wazima, maana utapia mlo huathiri ukuaji wa ubongo wa mtoto. Tatizo hili huwa kubwa pia kwa watoto ambao mama zao walikosa lishe bora wakati wa ujauzito. Na utafiti wa kisaikolojia unaonesha kuwa watoto ambao wamekulia katika familia zilizokuwa na mafarakano au magomvi, wengi wao huathirika kisaikolojia na pia huchangia kusababisha magonjwa ya akili. Watoto au kizazi kilichokulia katika mazingira ya vita, huweza kuongeza idadi ya watu wenye magonjwa ya akili au kuwa na taifa lililo na watu wasio na utu (cruelity) au vijana wasio na uwezo mzuri wa kuwa na mahusiano mazuri na jamii nyingine.
Mpendwa hili si suala dogo kama watu wengi wanavyofikiri. Maendeleo ya sayansi na teknolojia, utandawazi uliopo sasa, upatikanaji wa madawa ya kulevya umekuwa rahisi, sasa ukiyaweka mambo yote haya mbele ya kijana ambaye hakupata msingi mzuri wa maisha toka utotoni, kiafya na kiimani na asiye na neno la Mungu ndani yake kwa hakika ni rahisi sana jamii kumpoteza kijana huyu. Ila ninafurahi maana Mungu wetu kwa kweli ni mwema, maana yeye hutupa akili njema, hutupa ufahamu wa rohoni, hekima na busara hata kama tulikulia kwenye mazingira magumu. Hii ni kwa sababu Mungu hutuwazia mawazo ya amani na pia hutuinua uli tumtumikie yeye. Hivyo haijalishi kwamba ulizaliwa mazingira ya namna gani, Yesu anapokuwa upande wetu hufanya yote kuwa mazuri. Ukiwa kwa Yesu historia ya maisha yako haiwezi kuathiri maisha yako kamwe.

Ooh! Haleliya! Sikiliza, lengo la Ibilisi ni kuwafanya vijana wafanye dhambi na pia kuangamiza au kuteka vizazi vingi vijavyo. Vijana ni kundi kubwa na lina nguvu ya kufanya mabadiliko makubwa kiimani, kiuchumi, kisiasa na kijamii katika jamii yetu ya sasa, ikiwa vijana wataamua kubadilika na kumtafuta Mungu kwa bidii.

Haijalishi kuwa wewe ni mtoto, kijana au mzee kumbuka unayo nafasi yako muhimu unayopaswa kutumika kikamilifu sawasawa na mapenzi ya Mungu. Ninayo furaha kubwa sana ndani yangu kwa maana Mungu wetu yu mwema na hutupasha watumishi wake habari za mambo yajayo. Kwa hiyo ninaamini kuwa lipo kusudi kubwa tena maalum kwa Mungu kutufunulia siri hii kubwa.

Watumishi wa Mungu tuwe macho maana ipo kazi kubwa iliyopo mbele yetu kwa ajili ya utukufu wa Mungu, nayo ni kung’oa na kubomoa, na kuharibu ngome na kupanda.





JE YESU ANAIFAHAMU SIRI HII YA BOYFRIEND NA GIRLFRIEND?

Yesu aliuona uharibifu ambao Shetani aliufanya, wa kuharibu au kuvunja pendo la familia. Na ndiyo maana alipokuwa msalabani alisema hivi; ‘Mama tazama mwanao’ halafu akamwambia yule mwanafunzi, ‘Tazama mama yako’ Yoh 19;26-27 “Basi Yesu alipomwona mama yake na yule mwanafunzi aliyempenda amesimama karibu, alimwambia mama yake, mama tazama mwanao. Kisha akamwambia yule mwanafunzi, tazama mama yako. Na tangu saa ile mwanafunzi yule akamchukua nyumbani kwake” Yesu alipomwambia mama tazama mwanao na mtoto amtazame mama yake, maana yake, upendo wa ndani ya moyo (family love) ambao Ibilisi aliuharibu, uundwe, uumbike upya, uhuishwe tena. Biblia inaniambia yule mwanafunzi akamchukua mama yake nyumbani kwake. Maana yake ni hii; Ile nafasi ya moyo wa yule mwanafunzi, aliingia mama yake, na hii iliwezekana kwa neno la Yesu. Usiniulize kama yule mwanafunzi alikuwa ameoa au la, ninachojua ni kwamba Yesu alikuwa anahuisha upendo wa familia (family love)
Ndiyo maana wapendwa walio ndani ya Kristo kweli, na neno lake ndani yao , hawababaishwi na boyfriend au girlfriend maana ndani ya mioyo yao wamekamilishwa kwa neno la Kristo. Wengine watafikiri kwa kuwa wazazi wake au mzazi wake amefariki basi ni sawa kuwa na boyfriend au girlfriend, sivyo hata kidogo. Biblia inasema, Mungu wetu yeye ni Baba wa yatima. Maana yake nafasi za wazazi wako au mzazi wako inachukuliwa na Mungu mwenyewe.
Wengine wataniuliza, mbona nafasi ndani ya moyo wa Isaka haikuchukuliwa na Mungu? Kumbuka Isaka aliishi katika kipindi cha Agano la Kale na sisi tupo katika Agano Jipya, Mungu ametusogeza karibu sana na yeye katika Agano Jipya kuliko katika Agano la Kale. Kristo mwenyewe yupo ndani yetu tuaminio na kutii Yoh 15:4. Sikiliza; Hata kama family love itaharibiwa na Shetani, na wazazi kutowapenda watoto wao, amani, furaha na upendo wa Kristo huwahifadhi waliomwamini Yesu. Na hivyo hawatafuti amani au furaha au upendo kutoka kwa girlfriend au boyfriend bali kwa Yesu.
Hivyo ni dhahiri kabisa kuwa na (special relationship with opposite sex) girlfriend au boyfriend ni chukizo kwa Bwana. Soma maandiko vizuri, muombe Mungu akupe Roho ya mafunuo, akupe kujua na maandiko na macho ya moyo wako yatiwe nuru, ili uone njia ya Bwana ifaayo. Rumi 12:2 “Wala msiifuatishe namna ya dunia hii; bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema, yakumpendeza na ukamilifu” Hebu jiulize, hivi nikweli huwa unafahamu ukweli halisi au ni kwa sababu umekuta uhusiano wa namna hii upo na wewe ukaiga? Jiulize tena, hivi ni kweli Mungu ndiye anayekuongoza kuwa na special relationship with opposite sex? Kumbuka Biblia inakuambia, usifuatishe tu mambo ya dunia hii maana yake unapaswa kuyaelewa, nia yako igeuzwe, ifanywe upya ili usiyatamani mambo ya dunia bali uyatamani mambo ya Mbinguni. Pia ujue hakika mapenzi ya Mungu sio unabahatisha tu. Hivyo mpendwa usiige tu vitu mwombe Mungu akupe kujua.

SASA NIFANYE NINI?
Ndugu mpendwa ni vema ufahamu jambo hili ya kuwa pasipo Yesu huwezi kufanya neno lolote. Yoh 15:4b “…maana pasipo mimi (Yesu) ninyi hamwezi hufanya neno lolote” Maana yake ni hii; Hata sasa huwezi kufanya uamuzi ulio bora na sahihi katika kuwa na mahusiano kama hujajikabidhi kwa Yesu na kumruhusu aingie ndani ya moyo wako ili akuwezeshe kuwa na maisha yenye maamuzi sahihi na kufanya yampendezayo Mungu. Inawezekana upo katika uhusiano wa aina hiyo au ndiyo unaanza uhusiano huo. Najua unahisi kama utakosa vitu fulani vitamu na utakosa furaha, sikiliza furaha hiyo si ya kutoka kwa Bwana, hivyo ni vema utafute furaha kwa Yesu. Ikiwa wewe ni kijana mdogo acha kuyaamsha na kuyachochea mapenzi maana utavuna uharibifu kwa kuwa unapanda kwa mwili na sio kwa roho. Inawezekana pia wewe ni mzazi, kumbuka hakuna lisilowezekana kwa Mungu. Hata kama umechangia sana kuharibika kwa watoto au mtoto wako, ni vema ujinyenyekeze chini ya mkono wa Yesu, ulio hodari yeye atafanya sawasawa na haja ya moyo wako. Hakikisha unakuwa muda mzuri wa kuzungumza na familia yako.
Kabla ya kuendelea kukisoma kitabu hiki, ikiwa upo tayari kumpa Yesu nafasi ya kwanza katika maisha yako, na unasikia ipo hali ya kutaka kufanya yaliyo mema machoni pa Mungu, basi acha kujiuliza maswali ya upingamizi, acha kutazama au kufikiri juu ya huyo rafiki yako bali fikiri juu ya uhusiano wako na Mungu, omba sala hii kwa sauti ukimaanisha.
Bwana Yesu nakuja mbele zako, unitazame mwanao. Nimekutenda dhambi wewe. Ninatubu mbele zako, unisamehe na kuniosha dhambi zangu zote kwa damu yako. Ninavunja maagano yote niliyoyafanya na Shetani. Ninakuruhusu Roho Mtakattifu uingie ndani ya moyo wangu sasa. Uniongoze katika kweli yako. Ninaahidi kukutegemea wewe Yesu, na kukutumikia kwa uaminifu hata nitakapokufa. Asante Bwana Yesu kwa kuniokoa, niwezeshe kukufuata hata milele. Amina.
Ikiwa umeomba sala hii, dhambi zako zote zimefutwa, na Kristo yupo ndani ya moyo wako sasa, wala usitie shaka. Tangu sasa ni vema ushirikiane na wapendwa waliookoka na uwe ukisoma Biblia ili ukue kiroho. Usiache kumuomba Mungu maana sasa wewe ni mwanaye hivyo anakusikiliza kila umwitapo. Yoh 15:7 “Ninyi mkikaa ndani yangu na maneno yangu yakikaa ndani yenu, ombeni mtakalo lote nanyi mtatendewa” Siku zote utaendelea kuwa rafiki wa Mungu ikiwa utafuata maagizo ya Bwana na kuacha dhambi. Yoh 15:14 “Ninyi mmekuwa rafiki zangu, mkitenda niwaamuruvyo”
Jipe moyo utashinda maana Yesu naye alishinda. Ufunuo 3:11,21 “Kwa kuwa umelishika neno la subira yangu, mimi nami nitakulinda, utoke katika saa ya kuharibiwa iliyotayari kuujia ulimwengu wote kuwaharibu wakaao juu ya nchi. Naja upesi shika sana ulicho nacho asije mtu akaitwaa taji yako. Yeye ashindaye nitampa kuketi pamoja nami katika kiti changu cha enzi, kama mimi nilivyoshinda nikaketi pamoja na Baba yangu katika kiti chake cha enzi”
Ole wake apingaye neno la Mungu, maana hasira ya BWANA itakuwa juu yake

No comments: