Sunday, August 10, 2008

IJUE SIRI YA GIRLFRIEND NA BOYFRIEND -1

UTANGULIZI
Mwenendo wenu na uwe kama inavyoipasa injili ya Kristo, Wafilipi 1:27
Na ashukuriwe Mungu Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, yeye aliyeniwezesha kuandika kitabu hiki. Kitabu hiki kitakuwezesha na kukusaidia kuelewa undani wa Girlfriend na Boyfriend na kuona njia ipasayo ya uzima. Vijana wengi siku hizi huambiana nakupenda lakini hawajui nini maana halisi ya UPENDO au huambiana hivyo kiunafiki tu. Ni vema ufahamu utaratibu wa mapenzi jinsi ulivyopangwa na Mungu katika maisha yako. Maana huo utaratibu umewekwa ndani ya moyo wako tangu enzi, na wengi hawafahamu jambo hili. Muhubiri 3:11 “Kila kitu amekifanya kizuri kwa wakati wake tena ameifanya hiyo milele ndani ya mioyo yao , ila kwa jinsi mwanadamu asivyoweza kuivumbua kazi ya Mungu anayoifanya tangu mwanzo hata mwisho.

KWA NINI MUNGU AMEUMBA TOFAUTI ZA JINSIA?

Tendo la kujamiiana au tendo la ndoa limewekwa na Mungu mwenyewe kwa makusudi maalum na kwa utaratibu mzuri kabisa. Mungu hakuweka tofauti za jinsia kwa mwanadamu peke yake, bali pamoja na viumbe wengine. Lakini pana tofauti kubwa ya makusudi halisi ya kuweka tofauti kwa mwanadamu na kuweka tofauti hizo kwa viumbe wengine.

Mwanzo 1:20-25, “Mungu akasema maji nayajawe kwa wingi na kitu kiendacho chenye uhai, na ndege waruke juu ya nchi katika anga la mbingu… na kila ndege arukaye kwa jinsi yake. …Mungu akasema nchi na izae kiumbe hai kwa jinsi zake… na wanyama wa mwituni kwa jinsi zake ikawa hivyo”

Mungu anaposema kwa jinsi zake maana yake viumbe vyenye jinsia na namna tofauti. Aliumba namna hizo tofauti kwa NENO tu, lakini mwanadamu aliumbwa kwa neno (na tumfanye mtu kwa mfano wetu…) na kwa vitendo. Maana Mungu alimfanya mtu kwa mavumbi ya ardhi na akamfanya mwanamke kwa kutumia ubavu wa mwanamume. Uumbaji wa mwanadamu ni tofauti sana na viumbe wengine.

Viumbe wengine wote waliumbwa kwa jinsia na namna tofauti kwa ajili ya kuendeleza uumbaji (recreation) na pia kwa matumizi ya mwanadamu. Mojawapo ya sababu za kuumbwa kwa mwanamke na mwanamume ni;
Kuendeleza uumbaji wa Mungu
Kuvitawala vitu vyote
Kuitiisha nchi
Kusaidiana

Mwanzo 2:18, “Bwana Mungu akasema si vema huyo mtu awe peke yake, nitamfanyia msaidizi a kufanana naye” Wanyama hawakuambiwa hivi.

Mungu anapofanya kitu huwa na kusudi na utaratibu maalum wa alichokifanya. Tendo la ndoa liliwekwa na Mungu kwa makusudi maalum na aliweka utaratibu wake na malengo maalaum. Tendo la ndoa limekuwa chanzo cha matatizo mengi makubwa kwa mwanadamu si kwa sababu tendo la ndoa ni baya, ila ni kwa sababu watu wanalifanya nje ya wakati wa Mungu, na wanalifanya isivyotakiwa yaani kinyume na utaratibu na makusudi ya Mungu. Wengi huwa hawajui ya kuwa tendo la ndoa linatakiwa kufanywa kwa utukufu wa Mungu. Kwa mwanadamu tendo la ndoa huwaunganisha watu wawili wa jinsia tofauti kuwa mwili mmoja na huambatana na furaha ya hisia za ndani ambazo hukamilishwa kwa UPENDO. Ndiyo maana wavulana wengi wanapokuwa wakitongoza husema NAKUPENDA, ila siku hizi hata wasichana hutongoza. Hii ni kwa sababu upendo hukamilisha ndoa. Ndoa ni moja ya jambo ambalo Mungu amempa mwanadamu ili limpatie mwanadamu furaha na kamwe sio kwa ajili ya huzuni, hasira au matatizo. Lakini siku hizi ndoa imekuwa kama mwiba; maana watu wengi hudhani ndoa ni kama sehemu ya starehe na hawaichukulii ndoa kama sehemu ya kumtukuza Mungu.

Upendo chanzo chake halisi ni Mungu mwenyewe. Tangu enzo ya uumbaji Mungu alimpenda mwanadamu, na ndiyo maana mwanadamu alipoasi Mungu hakumwangamiza mara, bali alimwokoa na kuurejesha upendo halisi kwa njia ya Yesu Kristo. Katika Biblia Yesu ni Bwana arusi na kanisa ni Bibi arusi, na ndiyo maana kuna upendo wa ajabu wa Yesu kwa kanisa.

*********************************ENDELEA SEHEMU YA PILI ******************************

No comments: